Jumanne , 31st Dec , 2019

Waziri wa Fedha na Mipango Dkt Phiilip Mpango, ameeleza sababu iliyopelekea deni la Taifa kuongezeka kwa asilimia 11.7, kutoka Shilingi Trilioni 49.08 kwa mwezi Novemba 2018, hadi kufikia Trilioni 54.84 kwa mwezi Novemba 2019.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt Philip Mpango.

Waziri Mpango ameyabainisha hayo leo Disemba 31, 2019 Jijjini Dodoma, wakati akitoa taarifa ya hali ya Uchumi na utekelezaji wa Bajeti, ambapo amesema kuwa ongezeko hilo limetokana na uwepo wa riba ya mikopo ambayo mikataba yake iliingiwa zamani pamoja na ongezeko la mikopo mipya yenye masharti nafuu.

"Ongezeko la Deni limetokana na mambo mawili kwanza ni riba ya mikopo ambayo mikataba yake iliingiwa zamani, Pili ni mikopo mipya yenye masharti nafuu na ile ya kibiashara kwa ajili ya kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo, Serikali itahakikisha fedha tulizokopa zinatumika kujenga rasilimali zenye kuongeza msingi wa kuzalisha mali na uwezo wa kulipa mikopo hii" amesema Dkt Mpango.

Aidha Waziri Mpango amezitaka Taasisi 50 ambazo hadi sasa, hazijawasilisha michango yake kwa Serikali kwa muda muafaka kama alivyoagiza Rais Magufuli, wajiandae kuachia nafasi zao wenyewe.

"Hadi sasa bado mashirika na makampuni 50 ambayo hayajachangia, narudia kusisitiza kuwa Wenyeviti wa Bodi na wajumbe na wakuu wa Taasisi hizo 50, watekeleze maagizo la sivyo waondoke kwenye nafasi zao itakapofika saa 6:00 usiku, Januari 23, 2020" amesema Waziri Mpango.