Mwakinyo alivyoguswa na ajali ya mashabiki zake

Jumamosi , 30th Nov , 2019

Baada ya kuibuka mshindi dhidi ya mpinzani wake raia wa Mfilipino aitwaye Arnel Tinampay, Bondia Hassan Mwakinyo ameeleza kuguswa na tukio la ajali iliyowakumba mashabiki waliokwenda kumshangilia ambayo ilitokea eneo la Bunju jijini Dar es salaam.

Bondia Hassan Mwakinyo.

Katika ajali hiyo watu wawili wanatajwa kufariki Dunia huku taarifa za awali zikieleza majeruhi waliokuwa kwenye basi hilo walipelekwa kwenye Hospitali ya Bagamoyo.

Kupitia mtandao wa kijamii wa Instagram, bondia Hassan Mwakinyo ameandika kuwa,"kwanza nimshukuru mwenyezi mungu kwa kumaliza pambano langu salama,kwa dhati ya kipekee kabisa, naishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuwa bega kwa bega na mimi pamoja na Watanzania wote kwa ujumla wenu nawapenda sana pamoja na vyombo vya habari vyote"

"Pili nimeshtushwa na ajali iliyotokea jana usiku kwa mashabiki na ndugu zangu wa Tanga, walipokuwa wanatoka kwenye pambano langu, huzuni kubwa kwangu na Tanga kwa ujumla, nipo pamoja na familia na wana Tanga wote kipindi hiki cha huzuni, Allah awape kauli thabiti, na awape pepo ya firdaous innallilah wainnailaihi rajoun" ameongeza

Aidha katika pambano la jana ambalo alishinda kwa pointi  (97-93, 98-92, 96-96) lilihudhuriwa na baadhi ya wasanii mastaa  kama Ommy Dimpoz na Mwana Fa.