Jumatano , 11th Sep , 2019

Area 51' ni eneo linalopatikana huko Nevada, Marekani ni moja ya eneo ambalo linapewa ulinzi mkali sana na Serikali na hakuna mengi yanayojulikana kuanzia kinachofanyika au kinachoendelea katika eneo hilo, zaidi ya kutajwa ni eneo linalotumiwa na vikosi vya usalama kufanya majaribio ya

vifaa vya anga.

Eneo hilo limekuwa maarufu miongoni mwa watu wengi kutokana na kutajwa kuwa na uwepo wa Aliens (Viumbe wanaosemekana kuishi katika sayari nyingine), teknolojia ya hali ya juu ambayo imeletwa na hao viumbe na inasemekana wanafanya kazi na Serikali ya Marekani katika uundaji wa vifaa mbalimbali hususani silaha za kiteknolojia za hali ya juu.

Mwanzoni mwa mwaka huu kupitia mtandao wa Facebook watu walianzisha kampeni ya kuhamasisha kwenda eneo hilo kwaajili ya kuona kinachofanyika huko, Tukio hilo lilipewa jina la “Storm Area 51, They Can't Stop All Of Us” na ilipangwa kufanyika Septemba 20 mwaka huu kwa mtu yeyote anaejisikia kwenda huko ruksa kujumuika.

Serikali ya Marekani ilitangaza kuwa haina mpango wa kumdhuru mtu yeyote na kuwataka wote wanaopanga kwenda eneo hilo kutokufikiria kabisa kutaka kujua kinachoendelea sababu eneo hilo limewekwa ulinzi mkubwa ambao ni hatari kwa yeyote atakayejaribu kusogea karibu.

Mwanzilishi wa tukio hilo Matty Roberts pamoja na wenzake wameamua kukatisha tukio hilo huku wakilibadilisha na kuamua kulifanya kuwa tamasha ambalo litafanyika huko huko Nevada eneo la jangwa huku wakiahidi uwepo wa burudani ya kutosha kutoka kwa Wasanii mbalimbali.

Waandaaji hao wamewaonya watu ambao bado wana msisitizo wa kutaka kufika eneo hilo waache sababu wanahisi uvunjifu wa haki za kibinadamu unaweza kutokea kwa kiasi kikubwa kwa wote wataojaribu kwenda eneo hilo.

Tamasha limepangwa kuanza Septemba 19 mpaka 22, Kilichobaki ni kwako uamue kwenda kwenye tamasha au ulazimishe kwenda Area 51 ukakipate unachokitaka, kazi kwako.