Jumanne , 5th Apr , 2022

Uongozi wa klabu ya Yanga umethibitisha kuwa itawakosa nyota wake wa nne kwenye mchezo wa mzunguko wa 19 wa ligi kuu Tanzania bara dhidi ya Azam FC,mchezo utakaofanyika katika uwanja wa Azam Complex majira ya saa mbili na robo usiku mnamo April 6 mwaka huu .

Khalid Aucho kiungo wa Yanga.

Taarifa hiyo imethibitishwa na kocha msaidizi wa Yanga Cedrick Kaze kuwa nyota hao Faisal Salum, Khalid Aucho, Farid Mussa na Yannick Bangala wamepata majeraha na hivyo bado hawapo timamu kwa ajili ya mchezo huo

''Feisal na Aucho ni wanasumbuliwa na majeraha huku Farid aliugua ghafla jana na kukimbizwa hospitali, Yannic Bangala aliumia siku mbili zilizopita na hajafanya mazoezi na timu'' amesema Cerdick Kaze.

Kwa upande wa wenyeji wa mchezo huo Azam FC kupitia kwa kocha wa magolikipa Mwalo Hashim amesema licha ya Yanga kuwa bora na haijapoteza mchezo wowote wa ligi kuu lakini wao wamejipanga kuondoka na alama tatu kwenye mchezo wa kesho.
 

''Wachezaji wanajua umuhimu wa mchezo huu, kwahiyo tumejiandaa kushinda ili kuweza kufufua matumaini ya kuchukua ubingwa wa ligi kuu msimu huu'' amesema Mwalo Hashim.

Mchezo wa mzunguko wa kwanza walipokutana Uwanja wa Mkapa, Azam FC ilipoteza kwa kufungwa mabao 2-0 huku sasa Azam FC ikishika nafasi ya tatu kwenye msimamo wakiwa na alama 28 ilhali Yanga wakiwa kileleni na alama 48 katika michezo 19 waliocheza mpaka sasa.