Jumatano , 20th Dec , 2017

Klabu ya soka ya Azam FC imepata pigo tena kwa kumkosa mshambuliaji wake Mbaraka Yusuph ambaye anapelekwa nchini Afrika Kusini kwaajili ya matibabu ya majeraha aliyoyapata akiwa na timu ya taifa.

Msemaji wa Azam FC Jaffery Iddy Maganga amesema, baada ya Mbaraka kurejea nchini, daktari wa timu ya hiyo alifuatilia afya ya mchezaji huyo kwa vipimo vya hapa nchini na imeonekana kuwa hatoweza kuitumikia klabu yake mpaka pale atakapofanyiwa vipimo vikubwa nchini Afrika kusini pamoja na matibabu.

"Mtakumbuka Mbaraka Yusuph alikuwa na timu ya Taifa nchini Kenya katika michuano ya Challenge na kwa bahati mbaya akaumia na vipimo vimeonyesha ameumia sehemu ya goti na hawezi kucheza, tayari uongozi wa juu umetoa ruhusa kwa Mbaraka kupelekwa Afrika kusini kwaajili ya vipimo na matibabu”, amesema Maganga.

Hii ni mara ya pili kwa mshambuliaji huyo kuumia akiwa na timu ya Taifa ambapo mara ya kwanza aliumia katika michuano ya COSAFA iliyofanyika nchini Afrika Kusini mwezi Juni mwaka huu. Pia alipelekwa nchini humo kwa matibabu na klabu yake ya Azam FC.