Jumapili , 1st Mei , 2016

Klabu ya Azam fc imeweka wazi kuwa haijawahi na haitojaribu kuwazuia wachezaji wake wanaopata nafasi ya kutakiwa kwenda kujiunga ama kufanya majaribio katika timu yoyote nje ya nchi kwakuwa hiyo ni fursa ya maisha na maslai ya mchezaji na timu.

Winga wa kimataifa wa Tanzania, Farid Mussa akiwa mazoezini katika viwanja vya klabu ya Deportivo Tenerife.

Uongozi wa klabu ya Azam fc umesema haujawahi na hautofikiria kumzuia mchezaji yeyote wa timu hiyo kwenda kutumia fursa ya kujiunga na timu nje ya nchi ama kufanya majaribio ya kujiunga na timu yoyote nje ya nchi kwa kuwa kufanya hivyo ni kumnyima fursa mchezaji husika ya kusogea kimaisha lakini kimpira kwenda juu zaidi kimaslai.

Kauli ya Azam FC imetolewa na Afisa habari wa timu hiyo Jaffar Idd Maganga wakati akizungumzia maendeleo ya Winga wa kimataifa wa Tanzania, Farid Mussa ambaye kwa sasa yuko nchini Hispania alikokwenda kufanya majaribio na timu ya Daraja la kwanza ya Deportivo Tenerife.

Farid ambaye ameonekana kuwavutia viongozi wa timu hiyo tangu alipoanza mazoezi wiki moja iliyopita akijiunga na Wahispania hao moja kwa moja akitokea nchini Tunisia alikokwenda na timu yake ya Azam fc kucheza mchezo wa marudiano wa kombe la shirikisho barani Afrika (CAF Confederations Cup) tayari amekwishafanyiwa vipimo vya afya.

Jaffar amesema kinachoangaliwa katika usajili kwao kwanza ni mkataba wenye maslahi mazuri kwa mchezaji binafsi na pia malipo ya uhamisho yenye maslahi kwa timu yao ambayo ndiyo imemlea kwa gharama kubwa mchezaji husika.

Aidha Jaffar ametolewa mfano kitendo cha wao kumruhusu katikati ya ligi msimu uliopita mshambuliaji tegemeo wa timu hiyo ambaye pia ni nahodha wa timu hiyo John Bocco kwenda kufanya majaribio katika timu ya Super Sports United inayoshiriki ligi kuu ya Afrika kusini PSL lakini pamoja na kufuzu kilichomkwamisha Bocco si kunaniwa na wao Azam fc bali kitendo cha timu ya Super sports kutaka kumchukua mshambuliaji huyo kwa mkopo na wao Azam wakitaka ifanyike biashara ya mauziano ya moja kwa moja.

Jaffar Idd amesema awali kabla ya kiungo huyo kinda wa Azam FC, Farid Mussa kwenda huko Uhispania alitakiwa na moja ya vilabu vinavyoshiriki ligi kuu ya Ubelgiji lakini kutokana na maslahi yasioendana na mchezaji wala klabu hiyo ya Azam wakaona waiweke pembeni ofa hiyo na kuangalia ofa ya wakala ya kwenda Uhispania ambako nako awali iliripotiwa kuwa alitakiwa kwenda kufanya majaribio katika vilabu vikubwa viwili vya ligi kuu ya Uhispania La liga [Las Palmas na Athletic Bilbao] lakini kwa ushauri wa Wakala huyo na kuona ili Farid aweze kupata nafasi ya kucheza kwa haraka apate uzoefu na kujitangaza kirahisi akashauri ni vema mchezaji huyo aliyekulia katika kituo cha Azam fc akaanze kwa kucheza ligi ya pili kwa ukubwa nchini Hispania ya Hispania 'Segunda Division’ katika klabu ya Deportivo Tenerife ambako sasa kwa bidii kubwa kiungo huyo mwenye kasi anaendelea kupambana kuwania kupata nafasi ya kuichezea timu hiyo inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza.