Jumamosi , 2nd Jul , 2016

Mshambuliaji wa Real Madrid na nahodha wa Wales Gareth Bale sasa atakutana uso kwa uso na mchezaji mwenzake wa Real Madrid Cristiano Ronaldo baada ya usiku wakuamkia hii leo kuiwezesha timu yake kutinga nusu fainali ya michuano ya Euro 2016.

Moja ya hekaheka katika lango la Ubelgiji wakati wakishambuliawa na Wales.

Kikosi cha Wales kimetinga nusu fainali ya michuano ya Euro licha ya kuonekana ni wasindikizaji tu mwanzoni mwa michuano hiyo.

Wales inayoongozwa na Gareth Bale, imewatwanga masupa staa wa Ubelgiji kwa mabao 3-1 na kuushangaza ulimwengu.

Sasa katika hatua ya nusu fainali, Wales inakutana na Ureno inayoongozwa na Cristiano Ronaldo na yeye na Bale wote ni nyota wa Real Madrid.

Ikumbukwe wakati Bale akisajiliwa kwa dau la rekodi kutoka Spars kulikuwa na hali ya msuguano kati yake na Ronaldo ambaye naye alikuwa amesajiliwa misimu kadhaa iliyopita kwa kitita kikubwa ambacho kilikuwa rekodi wakati huo akitokea Manchester United kabla ya kunjwa rekodi hiyo na dau la Bale.

Ronaldo ambaye ni kipenzi cha mashabiki wa Real Madrid ilifika wakati akawa anahusishwa na kuondoka ndani ya klabu hiyo huku pia kwa nyakati tofauti ilisemekana kuhusika na tuhuma za kuwashawishi wachezaji wenzake kutompa ushirikiano wa kutosha Bale ili yeye aendelee kuwa ndiye mchezaji wa kipekee ndani ya Santiago Bernabiew na kunakipindi flani aliwahi kutoa matamshi kwa mashabiki akiwachochea kumchukia Bale ambapo baadae hali hiyo ilimalizwa na wawili hao kucheza kwa ushirikiano na kuisaidia timu yao kutwaa ubingwa wa ligi ya mabingwa barani Ulaya wakiwalaza mahasimu wao Atletico Madrid katika fainali iliyopigwa Mei mwaka huu jijini Milan Italia.

Pamoja na hali ya upinzani huo kumalizwa lakini suala la kukutana tena wakiwa katika majukumu tofauti ya kuziongoza nchi zao katika mchezo muhimu wa mtoano wa nusu fainali pengine kukaibua ushindani mwingine baina ya wachezaji hao wenye uwezo mkubwa katika soka kwa sasa ulimwenguni.

Robo fainali nyingine ya michuano hiyo inapigwa jumamosi hii usiku wakati Ujerumani inapokutana na timu ngumu na isiyotabilika ya Italia katika mchezo mgumu mno ambao mashabiki wengi wameupa jina la mchezo wa fainali kabla ya fainali kutokana na ubora na mbinu za vikosi vyote na matokeo yao hadi walipofikia hatua hiyo ndiyo yanatoa taswira ya ugumu wa mchezo huo.