Alhamisi , 6th Jan , 2022

Mchezaji namba mmoja kwenye mchezo wa Tenisi ulimwenguni, Novak Djovokic amezuiliwa kuingia nchini Australia, kwaajili ya kushiriki michuano ya wazi ya Australia ambayo yeye ndio bingwa mtetezi.

Novak Djokovic (pichani) katika moja ya mechi aliyopoteza

Katazo hilo kwa raia huyo wa serbia linatokana na tatizo lake la hati ya kusafiria aliyokata ambayo hairuhusu wageni ambao hawajapata chanjo ya UVIKO-19, kuingia nchini humo hii ikiwa ni siku mbili tu, tangu apewe ruhusu ya kushiriki mashindano hayo.

Baada ya sintofahamu hiyo, Djokovic na timu yake wamekata rufaa kwenye mahakama ya Shirikisho ya mzunguko ambapo itasikilizwa siku ya Jumatatu.

Djokovic bado hajaweka wazi hali yake kama amechoma chanjo ya UVIKO-19 au lah! Jambo ambalo linakwamisha utetezi wake wa taji hilo aliloshinda mara tisa.