Jumanne , 10th Jul , 2018

Baada ya michuano ya Sprite Bball Kings kupitia katika hatua za mchujo na 16 bora, hatimaye wikiendi ya Julai 7 na 8 zilipatikana timu zitakazocheza robo fainali na jana usiku ikachezeshwa droo ya kupanga mechi za hatua hiyo.

Kushoto ni Mkurugenzi wa Ufundi (BD) Goabert Msigati na kulia ni Alfred Makoye Kamishna wa waamuzi TBF, wakichezesha droo.

Moja ya timu ambazo zimetinga hatua hiyo ni mabingwa watetezi Mchenga Bball Stars ambao waliwafunga Oysterbay vikapu 117 kwa 56 katika hatua ya 16 bora, leo imepangwa kucheza na St. Joseph. Ikumbukwe kuwa bingwa atajinyakulia milioni 10, mshindi wa pili milioni 3 na milioni 2 kwa MVP.

Katika droo hiyo ambayo ilikuwa inaruka moja kwa moja kupitia East Africa Television na East Africa Radio chini ya usimamizi wa maafisa wa shirikisho la Kikapu nchini TBF, ilishuhudiwa ikizikutanisha timu za Temeke Heroes dhidi ya Portland katika mchezo mwingine unaotarajiwa kuwa na ushindani mkubwa.

Mechi nyingine ya robo fainali ni kati ya Water Institute ambao waliwashangaza Raptors kwenye mchezo wa 16 bora kwa kutokea nyuma kwa takribani vikapu 20 na kushinda kwa vikapu 77 kwa 66, wamepangwa kucheza na Flying Dribblers.

Wawakilishi wa timu 8 zilizofuzu robo fainali wakifuatilia droo kwa makini.

Aidha droo hiyo ambayo pia ilishuhudiwa na wawakilishi wa timu hizo 8, imewakutanisha wakali wengine ambao ni Team Kiza dhidi ya DMI. Mechi hizo za robo fainali ya Sprite Bball Kings inayoandaliwa na East Africa Television LTD chini ya udhamini wa kinywaji cha Sprite, zitachezwa wikiendi ya Julai 21. Endelea kufuatilia vipindi vyetu hivi karibuni utajulishwa uwanja ambao utatumika kwenye mechi hizo.