Jumatano , 27th Dec , 2017

Mshambuliaji wa Tottenham Harry Kane amesema kitendo cha kufananishwa na wachezaji  kama Lionel Messi na Cristiano Ronaldo ni jambo kubwa maishani kwake na ataendelea kuhakikisha anakuwa bora siku hadi siku.

Kane mwenye umri wa miaka 24 jana aliipiku rekodi ya mkongwe Alan Shearer ya mabao 36 kwa kufikisha mabao 39 ndani ya mwaka mmoja katika ligi kuu soka nchini England.

“Najisikia vyema kuwa na mwaka mzuri namna hii, nitaendelea kujituma ili niwe bora zaidi kila siku katika kazi yangu ya soka”, amesema Kane.

Kuhusu kufananishwa na nyota wawili Messi wa Barcelona na Ronaldo wa Real Madrid, Kane amesema ni jambo zuri kwake na inaonesha jinsi gani ubora wake unaendelea kukua kila siku.

Hivi sasa Kane ndiye mchezaji mwenye mabao mengi zaidi kwa mwaka 2017 akiwa na mabao 56 akiwazidi Messi mwenye mabao 54 na Ronaldo mwenye mabao 53.