Jambo atakaloanza nalo bosi mpya Simba

Jumanne , 10th Sep , 2019

Afisa Mtendaji Mkuu mpya wa klabu ya Simba, Senzo Mazingiza amebainisha wazi kuwa atahakikisha klabu hiyo inafanya usajili wa kitaalamu katika dirisha dogo Desemba ili kuiwezesha klabu hiyo kutetea ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania bara.

Afisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Senzo Mazingiza

Mazingiza ambaye ni raia wa Afrika Kusini ameteuliwa katika nafasi hiyo baada ya kuwashinda wenzake saba waliokuwa wanachuana katika nafasi hiyo ambayo iko wazi baada ya, Crescentius Magori kumaliza muda wake.

Ikiwa ni wiki ya kwanza katika nafasi hiyo, amesema kwamba atahakikisha anasimamia vizuri suala la usajili ndani ya kikosi kwa kuwaleta wachezaji ambao watakuwa na viwango vikubwa.

Najua Simba ni timu kubwa na yenye malengo mapana, sasa ni lazima mambo yaende kiuwazi wa juu na kisomi pia. Najua kunahitajika nguvu kubwa ya wachezaji ambao wataisaidia timu kwenye ligi, hasa baada ya kuondoshwa katika Ligi ya Mabingwa Afrika".

Nitasimamia suala la usajili kuona Simba inapata wachezaji wa juu ambao watakuwa na uwezo, kuhakikisha kuwa inatwaa ubingwa wa ligi kwa mara nyingine tena,” amesema Mazngiza.

Simba hivi sasa inashiriki katika mashindano ya Kombe la Shirikisho na Ligi Kuu Tanzania Bara pekee, tofauti na malengo ambayo ilijiwekea kabla ya msimu kuanza, ambapo wachezaji wengi wakubwa walisajiliwa kwa lengo kuu la kufika hatua kubwa katika mchuano ya Klabu Bingwa Afrika.