Jumatano , 9th Dec , 2020

Ligi kuu soka Tanzania Bara inatazamiwa kuendelea tena hii leo kwa michezo miwili ya viporo ya mzunguko wa 12 kwa vilabu vya Simba na Namungo waliokuwa wanawakilisha nchi kwenye michezo ya kuwania kufuzu michuano ya kimataifa Barani Afrika.

Kocha wa Simba, Sven Vandenbroeck (kushoto) akimkabidhi jezi Luis Miquissone (kulia) kipindi alipokua akijiunga na miamba hiyo ya soka hapa nchini Tanzania.

Mabingwa watetezi Simba watajitupa dimbani dhidi ya Maafande klabu ya Polisi Tanzania kwenye dimba la Mkapa mishale ya saa 1:00 Usiku ilhali Namungo wamesalia mkoani Lindi kuwakaribisha klabu ya Biashara United Mara saa 10:00 kamili jioni kwenye dimba la Majaliwa.

Kuelekea kwenye mchezo wa Simba dhidi ya Polisi TZ unaosubiriwa na wafuatiliaji wengi wa soka nchini, Kocha wa klabu ya Simba Sven Vandebroeck amethibitisha kuwakosa nyota wake Rally Bwalya mwenye matatizo ya kifamilia, Joash Onyango mwenye majeraha ingawa amujuza uma kwamba  Chris Mugalu amereja kikosini.

Mchezo huo umeibua hisia za wapenzi na wafuatiliaji wa mpira wa miguu nchini kwa kile wanachosubiri kuona kama kocha wa Simba Sven ataingia na mpango kazi maalum wenye kuifanya timu yake iweze kucheza na kutengeneza nafasi nyingi za mabao dhidi ya Polisi TZ inayocheza kwa kujilinda zaidi, jambo ambalo limeonekana kama ni changamoto kubwa kwa kocha huyo wa Ubelgji.

Maoni ya Abissay Stephen Jr juu ya Plan B ya Simba

Kocha wa Simba Sven Vanderbroeck anapata wakati mgumu sana wa kuifanya timu yake icheze na kutengeneza nafasi za wazi na kufunga mabao yatakayowafanya washinde mchezo akicheza dhidi ya timu zinazojilinda sana kwa idadi kubwa kwenye lango lao “Kupaki bus” au “ Low Block”.

Mbinu zipi kiufundi zinazofaa kucheza na timu inayocheza kwa kujihami? Kiufundi, kutumia sana winga wenye uwezo mkubwa wa kuwatoka walinzi na kujitengenezea nafasi wenyewe, kutumia viungo wenye uwezo mkubwa wa kufunga kwa umbali mrefu na kutumia pasi ndefu zenye shabaha kwa washambuliaji.

Mbinu nyingine ambayo hutumika ni kucheza pasi nyingi kwenye lango lako ili kumtamanisha mpinzani wajisahau na waje kwenye lango lako wakifikiri wakija wengi wataupata mpira karibu na lango lako na kufunga kirahisi, kwenye hili Simba wanajitahidi sana.

Changamoto ninayoiona ni Simba kukosa wacheza wengine wengi wenye sifa za kucheza Plan B dhidi ya timu inayojihami na kumpa ugumu kocha wake mara nyingi.

Ukimuondoa Said Hamis Ndemla na Jose Luis Miquissone, wachezaji kwenye safu ya kiungo na uchambuliaji naona hawaendani na plan B.

Said Hamis Ndemla anauwezo mzuri wa kupiga pasi ndefu na kufunga mabao kwa umbali mrefu lakini hapati nafasi ya kucheza mara kwa mara.

Luis Miquissone anao uwezo mzuri wa kuwatoka walinzi kuwatengenezea nafasi wenzake na yeye kufunga mabao ndiyo maana ametengeneza mabao 4.

Ibarahim Ajib anaweza kupiga pasi ndefu ila hapigi nje ya boksi, Jonas Mkude sio mpigaji na muda mwingi anacheza mbali na lango la mpinzani, Clatous Chama na yeye ni vile vile, Mzamiru Yasini sio mpigaji, Benard Morrison hayupo kwenye utimamu mzuri, hachezi kwa ajili ya kushindana licha ya kuwa angefaa.

Sasa matokeo yake ni kocha kushindwa kuwapata wachezaji wengine viungo wengi wanaopiga umbali mrefu na washambuliaji wenye kasi kuendana na plan B.

Nahodha John Bocco, Chris Mugalu na Meddie Kagere MK14 wote hawana kasi za kuwasaidia kucheza mipira mirefu  ambayo ingetengenezwa na viungo wa Simba.

Kocha Sven anaowajibu wa kusaka ubora kwa wachezaji wake wachache wamfae kwenye Plan B. au kubadili mfumo wa kiuchezaji ili kupata kilichobora kwa wachezaji alionao.

Mara nyingi, Sven amekuwa akifanya mabadiliko ya wachezaji wanaocheza katika nafasi zinazoshabihiana, kana kwamba aliyopo ndani ya uwanja amechoka, anahitaji msaada wa mwenzake, lakini sio kubadili kiufundi ambayo italeta utofauti wa kiuchezaji.