"Lazima tukubali wenzetu wako vizuri" - Mkwasa

Jumapili , 5th Jan , 2020

Kocha wa Yanga, Boniface Mkwasa amesema kuwa alikuwa na wakati mgumu baada ya kufungwa mabao mawili kwenye mchezo dhidi ya watani wao Simba.

Kocha wa Yanga, Charles Boniface Mkwasa

Mchezo huo uliopigwa katika uwanja wa taifa ulimalizika kwa sare ya mabao 2-2, Simba ilikuwa ya kwanza kupata bao kipindi cha kwanza kupitia kwa Meddie Kagere kwa mkwaju wa penalti kabla ya kuongeza la pili dakika za mwanzo za kipindi cha pili, Yanga ilirudisha mabao yote kipin di cha pili kuptia kwa Mapinduzi Balama na goli la kujifunga la Mohamed Hussein.

Mkwasa amesema kuwa ulikuwa ni wakati mgumu kwao baada ya kufungwa mabao mawili lakini aliongeza morali kwa wachezaji na kupelekea kurudisha mabao yote.

"Lazima tukubali wenzetu wamekaa pamoja kwa muda mrefu na wanacheza kwa pamoja lakini na sisi pia ndio tunajaribu kukaa pamoja kutengeneza timu yetu. Kusema kweli nilikuwa na wakati mgumu sana baada ya kufungwa goli mbili nikaona inaweza kuwa shida", amesema Mkwasa.

"Ulikuwa ni mchezo mgumu na ni moja kati ya mchezo bora kati ya Simba na Yanga bila kuwa na ushabiki wala masuala ya Kiswahili swahili na nadhani wlaiokuja wote wamefurahi", ameongeza.

Kwa upande wa kocha wa Simba, Sven Vanderbroeck amesema kuwa walifungwa mabao mawili kipindi ambacho walikuwa pungufu ndani, wakitibu majeraha nje ya uwanja lakini baada ya muda walirudi katika hali ya kumiliki mpira.

Baada ya mchezo huo, sasa Simba inaongoza ligi kwa pointi 35, Yanga ikiwa nafasi ya nne kwa pointi 25.