Jumanne , 27th Nov , 2018

Baada ya tetesi kueelezwa kuwa mabosi wa Yanga wameanza mazungumzo ya kimyakimya na beki kitasa wa Lipuli FC, Ally Sonso, uongozi wa Lipuli FC umeibuka na kusema kuwa haijafanya mazungumzo yoyote na Yanga juu ya mchezaji huyo.

Kikosi cha Lipuli FC

Beki huyo ambaye ni tegemeo ndani ya kikosi cha Lipuli, ameingia katika rada za Yanga ikiwa mpaka sasa dirisha dogo la usajili likiwa wazi. Licha ya tetesi za kumsajili beki huyo kushika kasi, uongozi wa Lipuli umesema kuwa mchezaji huyo ni mali yao na suala la kumuuza mchezaji Ally Sonso ni tetesi tuu kama zilivyo tetesi zingine.

Akizungumza na www.eatv.tv, Afisa Habari wa Lipuli FC, Clement Sanga amesema, "Hizo ni tetesi tuu kama ambavyo umesema, sisi kama klabu hatujapata taarifa yoyote kutoka Yanga kumtaka mchezaji wetu Ally Sonso".

"Mpaka sasa tuendelee kuziona ni tetesi mpaka hapo zitakapobadilika na kuwa mambo kamili, kwa sasa hatuwezi kuzungumzia chochote, kama kuna maazimio yoyote kuhusu mchezaji wetu basi mimi ndiyo msemaji wa klabu hii, kwahiyo nitatoa taarifa rasmi kwasababu huyu mchezaji ni mali ya Lipuli FC na wala si mali ya mtu," ameongeza.

Wakati hayo yakiendelea, kocha mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera amesema kuwa kwa upande wake haoni haja ya kuongeza mchezaji mpya kwa sasa kwakuwa klabu ya Yanga ina matatizo ya kiuchumi.

"Haiwezekani nyumbani kwako kuna matatizo, mtoto wako haendi shule halafu unakwenda kumchukua mtoto wa dada yako na kumleta nyumbani, siwezi kuhitaji mpya wakati zaidi ya wachezaji 10 wananililia ili wapate nafasi," amesema.