Jumapili , 8th Jul , 2018

Katika mwendelezo wa mechi za hatua ya 16 bora kutafuta timu 8 zitakazocheza robo fainali, Mabingwa watetezi wa michuano ya Sprite Bball Kings, Mchenga Bball Stars wameanza kampeni za kutetea ubingwa wao kwa kutoa kipigo tishio.

Timu ya Mchenga Bball Stars ambnao ni mabingwa watetezi wa Sprite Bball Kings

Katika mchezo ambao umemalizika asubuhi hii kwenye uwanja wa Bandari Kurasini, mabingwa hao watetezi wameipa kipigo cha vikapu 117 kwa 56 timu ya Oysterbay, hivyo kuanza vizuri mbio za kutetea ubingwa pamoja na kusaka milioni 10 zingine ambazo huwa ni zawadi ya bingwa.

Mchenga Bball Stars leo wameonekana na sura mpya kama Jonhson Mohamed ambaye amefunga vikapu 21, Christian Joseph vikapu 23 huku Baraka Sadick akifunga vikapu 16. Ikumbukwe kuwa Mchenga wanashiriki michuano hii bila ya nyota wao  Rwehabura Munyagi ambaye aliibuka (MVP) kwa mwaka 2017.

Kwa upande wa wachezaji waliokuwepo msimu uliopita Massero Nyirabu, amefunga vikapu 26 na kuchukua 'rebound' 10 na 'ku-assist' mara tatu katika mchezo wa leo ambao ni wa kwanza kwa mabingwa watetezi baada ya wao kupita moja kwa moja bila kucheza mechi za mchujo.

Mchenga na washindi wengine watatu wa leo wanaungana na timu za Portland, Flying Dribblers, DMI na St. Joseph ambazo jana zilikata tiketi ya kucheza robo fainali.