Jumanne , 28th Jun , 2016

Sasa ni rasmi mabondia wawili wa ngumi za kulipwa nchini waliojitokeza kuungana na ngumi za ridhaa kwa ajili ya Olimpiki ndiyo wataiwakilisha nchini katika michuano ya kuwania tiketi ya kushiriki michuano ya Olimpiki huko Venezuela.

Bondia Thomas Mashali.

Shirikisho la Ngumi nchini Tanzania BFT limesema mabondia wawili wa ngumi za kulipwa Amos Mwamakula na Thomas Mashali walioingia katika ngumi za ridhaa ili kushiriki michuano Olimpiki ndiyo wataelekea nchini Venezuela.

Rais wa BFT Muta Rwakatale amesema mabondia hao wote wako vizuri na tayari taratibu zao za safari kuelekea nchini Venezuela zimekamilika.

Muta ambaye ni bondia wa wazamani wa ngumi za ridhaa amesema baada ya kupata maombi ya nia thabiti ya mabondia hao kuonyesha uzalendo yakutaka kuiwakilisha nchi katika michuano hiyo mikubwa wao kama shirikisho BFT na kwakufuta agizo la chama cha kimataifa cha ngumi duniani AIBA kupitisha sheria ya mabondia wa kulipwa kuingia ngumi za ridhaa yaani [amature pro boxing] wakaona ni vema wawape nafasi hiyo na kimsingi wamefuatilia na kurizika na maandalizi ya mabondia hao na wanaimani wataenda kufanya vema na kufuzu kuelekea nchini Brazil kutakofanyika fainali zenyewe za Olimpiki jijini Rio.

Aidha, Muta amesema mabondia hao watakaporudi wataungana na mabondia wengine wawili wa ridhaa Suleiman Kidunga na Swanga ambao watakwenda katika mashindano hayo kwa nafasi ya upendeleo kutokana na Tanzania kukosa mabondia waliofuzu moja kwa moja kupitia ushiriki wa michuano ya kufuzu.

Akimalizia Muta amesema pia kocha Mkenya ambaye ana sifa za nyota tatu kama ilivyoagizwa na kanuni za kamati ya kimataifa Olimpiki IOC za kuwaongoza mabondia katika mashindano hayo ataungana moja kwa moja na timu hiyo kwa maandalizi ya muda mfupi na baadaye kuelekea Rio Brazil kwa ajili ya fainali hizo zitakazopigwa mwezi Agosti.