Jumatano , 18th Mar , 2015

Mashindano ya Klabu Bingwa ya Tanzania Bara na Visiwani yanatarajia kuanza Machi 20 mpaka 21, Bwawa la kuogelea la shule ya Kimataifa iliyopo Tegeta jijini Dar es salaam kwa kushirikisha vilabu 15 vya Tanzania an Zanzibar.

Akizungumza na East Africa Radio, Katibu Mkuu wa Chama cha Kuogelea nchini TSA Noel kihunsi, amesema mashindano hayo yatashirikisha muogeleaji mmoja mmoja kuanzia miaka tisa mpaka 15 ambapo kwa upande wa makundi watashiriki kuanzia miaka tisa mpaka 10, 10-11,11-12,12-13,13-14 na 14-15 na 15 na kuendelea ambayo ni huru kwa mtu yeyote kushiriki.

Kihunsi amesema, mashindano hayo yatashirikisha umbali mbalimbali kuanzia mita 50, 100, 200, 800 na kuendelea huku ikishirikisha mitindo minne ya kuogelea.

Kihunsi amesema, timu shiriki katika mashindano hayo zitaanza kuwasili kuanzia kesho kwa ajili ya kufanya mazoezi ya mwisho katika bwawa hilo ili kuweza kupata uzoefu katika Bwawa hilo kwa kila mshiriki ili kuweza kufanya vizuri.

Kihunsi amesema, mashindano hayo yatasaidia kuweza kupata timu itakayoweza kushiriki mashindano mengine mbalimbali ya ndani na nje ya nchi.