Jumatano , 14th Apr , 2021

Mabingwa watetezi wa ligi kuu Tanzania bara, Wekundu wa msimbazi Simba wanatazamiwakuanza kucheza michezo yao ya viporo dhidi ya Mtibwa Sukari saa 10:00 jioni ya leo April14,2021 kwenye dimba la Mkapa huku kocha wake msaidizi Selemani Matola akitamba kuibuka na alama tatu.

Kocha msaidizi wa Simba, Selemani Matola.

Matola amesema “Tumejipanga kuona tunapata matokeo mazuri, jeuri tuliyonayo ni kwamba kikosi chetu chote kipo imara, hakuna majeruhi na wachezaji wote wamefanya mazoezi ni uamuzi wa wetu kuamua yupi acheze katika mchezo wa huo”.

Kwa upande wa kocha wa makipa wa Mtibwa Sukari, Sudy Slim amesema Mtibwa wamejiandaa vizuri kucheza na mabingwa hao huku akiweza wazi hali za baadhi ya wachezaji nyota wa kikosi hicho.

“Salum Kihimbwa amekosa mechi 15 kutokana na majerha ya muda mrefu hivyo hatokuwepo, Jafari Kibaya alikosa mechi 11 lakini amerejea na alicheza mchezo uliopita dhidi ya Azam, Boban Zirintusa alikuwa nje kwa mechi 12 huenda akarejea tunasubiria ripoti ya daktari”.

(Kocha wa Makipa wa Mtibwa Sukari, Sudy Slim.)

Kuhusu taarifa rasmi ya kuondoka kwa aliyekuwa kocha wake mkuu, Mrundi, Hitimana Thierry, nahodha wa Mtibwa, Issa Rashid 'Baba Ubaya' ameweka wazi kuwa kocha huyo si wa klabu hiyo tena.

“Kikubwa tunamshukuru kwanza mwalimu tuliyenaye sasahivi ameshaiweka saikolojia ya wachezaji vizuri, kuhusu mwalimu aliyeondoka tuseme sisi tumeshasahau kuhusu uondokaji wake, tunachofanya ni kupigania kuona tunaitoa timu hapa ilipo”.

Simba ipo nafasi ya tatu, ikiwa na alama 46 baada ya kucheza michezo 20 ilhali Mtibwa Sukari ipo nafasi ya 15 ikiwa na alama 24 baada ya michezo 23. Na kama Simba ikiibuka na ushindi basi watafikisha alama 49, utofauti wa alama 2 na vinara Yanga na michezo 3 nyuma.