Jumanne , 4th Jul , 2017

Droo ya nne na ya mwisho ya kupanga ratiba ya michuano ya kikapu ya 'Sprite BBall Kings' imefanyika usiku wa kuamkia leo Jijini DSM kwa usimamizi wa Shirikisho la mpira wa kikapu Tanzania {TBF} kushirikiana na EATV LTD pia kushuhudiwa na timu shiriki

Mkuu wa vipindi vya East Africa Radio Nasser Kingu (Kushoto) na mtangazaji wa EATV, Suzy, wakiendesha droo ya nne kupanga ratiba ya michuano ya Sprite BBall Kings iliyofanyika usiku wa kuamkia leo.

Michuano hiyo itashirikisha timu nne (4) ambazo ni Kurasini Heat, TMT, Flying Dribblers pamoja na Mchenga BBall Stars pekee zilizoweza kufuzu hatua ya robo fainali kwa kuwafunga wapinzani wao mchezo uliyochezwa siku ya Jumamosi katika viwanja vya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Akizungumza wakati wa zoezi hilo, mkuu wa vipindi vya East Africa Radio Nasser Kingu, amesema mechi hizo zitachezeshwa tofauti na ilivyokuwa katika mzunguko wa mtoano pamoja na robo fainali ulivyokuwa.

"Hongereni kwa kuingia hatua ya nusu fainali, mechi zinazofuata zitachezwa kwenye Julai 15, 22 na 29 mwaka huu, tumefanya hivyo ili tuweze kuwapa muda mzuri wa kufanya maandalizi yenu katika mapambano pia kuhusu suala la uwanja litatangazwa muda si mrefu, nawaomba mfuatilie na kuangalia EATV na kusikiliza East Africa Radio bila ya kusahau 'social network' zetu ili muweze kupata 'update' zote", alisema Nasser.

       Wawakilishi wa timu mbalimbali waliohudhuria kushuhudia droo ya wazi ya nne michuano ya Sprite BBall Kings.

Kwa upande mwingine, mshindi wa kwanza wa mashindano hayo anatarajiwa kuondoka na kitita cha shilingi milioni 10 akifuatiwa na mshindi wa pili kupata milioni tatu bila ya kumsahau mchezaji bora {MVP} kuondoka na shilingi milioni mbili.