
Mkataba wa Messi Barcelona unamalizika Juni 2021
Kujiuzulu kwa Bartomeu katika nafasi ya Urais ndani ya FC Barcelona inatajwa kuwa ni sababu inayoweza kumfanya Lionel Messi kusalia katika kikosi hicho cha mabingwa wa ulaya mara 5 na kusaini mkataba mpya.
Messi mwenye umri wa miaka 33 aliomba kuondoka Barcelona kabla ya msimu huu wa 2020/21 kuanza lakini ameendelea kusalia klabu hapo na inaripotiwa mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Argentina ataondoka mwisho mwa msimu huu baada ya mkataba wake kumalizika.
Moja ya sababu ya Messi kuomba kuondoka ilikuwa ni kutoridhishwa na utendaji wa bodi ya klabu hiyo chini ya utawala wa Bartomeu.
Mchezaji huyo bora wa Dunia mara 6 ameshinda mataji 10 ya ligi kuu Hispania La liga, ubingwa wa ligi ya mabingwa ulaya mara 4 akiwa na kikosi cha Barcelona. Vilabu vya Manchester City ya England na Inter Milan ya Italia vimeonyesha nia ya kumsajili Lionel Messi.