Alhamisi , 30th Dec , 2021

Aliyekuwa kipa wa Mtibwa Sugar, Aboutwalib Msheri sasa rasmi ni mali ya Yanga baada ya viongozi wa Jangwani kukamaliza na Mtibwa Sugar.

Msheri alisaini mkataba wa kuitumikia Yanga kwa miaka mitatu jana Jijini Dar es Salaam dakika chache baada ya kufika akitokea Tanga alikofuatwa na Yanga.

Mechi kati ya Mtibwa Sugar na Coastal Union iliyopigwa Jumanne na Msheri kuonesha kiwango bora zaidi akiisaidia timu yake kushinda bao 1-0 ugenini Tanga ndiyo ilikuwa ya Mwisho kwa kipa huyo kulidakia chama lake hilo la tangu utotoni.

Awali dili hilo liliingia ugumu baada ya viongozi wa Mtibwa kukataa kumuuza Msheri wakidai kuwa ni mchezaji tegemeo kikosini hapo hivyo hauzwi kwa gharama yeyote ile.

Baada ya hapo Msheri aliomba kuvunja mkataba kwani alikuwa tayari na mipango ya kujiunga Yanga na akawa tayari kutoa Sh 20 milioni kuvunja mkataba wa mwaka mmoja na nusu uliokuwa umebaki ndipo vigogo wa Mtibwa wakastuka na kuwaita mabosi wa Yanga mezani wakazungumza na kukubali kuwauzia kipa huyo.