Ijumaa , 12th Mar , 2021

Mcheza kikapu wa timu ya Miami Heat, Meyers Leonard amepigwa faini ya dola 50, 000 za kimarekani ambazo ni sawa na milioni 115, 950, 000 za kitanzania kwa kukutwa na kosa la kutumia maneno ya kibaguzi dhidi ya jamii ya watu wa kiyahudi.

Mchezaji wa Miami Heat, Meyers Leonard.

Meyers alirekodi video siku ya jumatatu akiwa anacheza game huku akitoa maneno ambayo yalithibitika kuwa ya kibaguzi iliyosambaa sana kwenye mitandao ya kijamii na mpaka kufikia usiku wa jana ndipo akawekwa hatiani.

Mbali na faini ya mamilioni hayo ya fedha, Meyers amefungiwa kwa muda wa wiki moja licha ya kuwa nje ya uwanja mpaka mwisho wa msimu kutokana na maumivu ya bega yanayomsumbua.

Mkurugenzi wa Shirikisho la mpira wa kikapu nchini Marekani, Adam Silver amesema “Maneno ya Leonards yalikuwa hayana utetezi na yanaumiza sana, maneno yenye mashambulizi kama haya hayana nafasi kwenye NBA na kwenye jamii yetu”.

“Tumewasiliana na Meyers kwamba, maneno kama yale hayatovumilika kwasababu yatavua thamani ya ligi yetu. Muda wote tupeleke mbele usawa, uvumilivu, umoja na heshima”. Aliongezea Silver.

Baada ya kupata taarifa za makosa yake, Meyers aliomba radhi kwa kusema “Nina kiri kufanya makosa na siwezi kujificha kwenye kitu kinachoumiza kwa mtu mwingine. Hivi siyo maana halisi ya jinsi nilivyo”

Timu ya Meyers, Miami Heats inataraji kucheza mchezo wa NBA dhidi ya Chicago Bulls saa 11:00 alfajiri ya kuamkia kesho jumamosi ya tarehe 12 machi 2021.