Jumatatu , 2nd Mei , 2016

Kwa mara nyingine tena kama ilivyozoeleka haipiti wiki ama michezo kadhaa bila ratiba ya ligi kuu ya soka Tanzania bara kurekebishwa kwa kufanyiwa marekebisho madogo kwa baadhi ya michezo ama kuahirishwa kutokana na sababu wanazojua bodi ya ligi.

Kikosi cha mabingwa watetezi wa ligi kuu ya soka Tanzania bara VPL msimu wa 2015/2016 Yanga SC.

Mchezo wa Ligi Kuu ya soka Tanzania Bara kati ya Ndanda FC ya Mtwara na Young Africans umerudishwa nyuma kwa siku moja na sasa utachezwa Mei 14, mwaka huu badala ya Mei 15, kama ratiba ya awali inavyosomeka.

Taarifa ya Bodi ya Ligi Kuu ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) imesema sababu za kurudisha nyuma mchezo huo Na. 218 utakaofanyika Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara ni kuipa timu ya Young Africans nafasi ya kujiandaa na kusafiri kwenda nchini Angola kwenye mchezo wa kimataifa wa Kombe la Shirikisho Barani Afrika dhidi ya Esperanca ya huko.

Mbali ya mechi hiyo, kuna michezo miwili ambayo imesogezwa mbele pia kwa siku moja. Mechi hizo ni kati ya Simba na Mwadui mechi ambayo sasa itachezwa Mei 8,mwaka huu badala ya Mei 7.

Sababu za mchezo huo kusogezwa mbele ni kwamba Mei 7, mwaka huu kutakuwa na mchezo wa kimataifa utakaozikutanisha Young Africans dhidi ya Esperanca ya Angola kuwania Kombe la Shirikisho.

Mchezo mwingine uliosogezwa mbele ni kati ya Kagera Sugar dhidi ya Azam FC ambao sasa utafanyika Mei 8,mwaka huu badala ya Mei 7.

Sababu za mchezo huo kusogezwa mbele ni Uwanja wa Kambarage Shinyanga Mei 7,mwaka huu uwanja huo utakuwa na mchezo kati ya Stand United ya Shinyanga dhidi ya Coastal Union ya Tanga.

Kadhalika Ligi Kuu Tanzania Bara, inatarajiwa kuendelea kesho Mei 3,mwaka huu kwa mchezo mmoja ambao mabingwa watetezi Young Africans ya Dar es Salaam itakuwa ugenini dhidi ya wenyeji wao Stand United chama la wana katika mchezo muhimu kwa Yanga utakaopigwa kwenye Uwanja wa Kambarage, Shinyanga.

Jumatano Mei 4,mwaka huu Azam FC ya Dar es Salaam itakuwa mwenyeji wa JKT Ruvu ya Pwani kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.