Ijumaa , 22nd Oct , 2021

Mabingwa watetezi wa ligi kuu, klabu ya Simba imefanikiwa kuzoa tuzo nyingi, tuozo 6 kwenye hafla ya utoaji tuzo ambayo ilifanyika usiku wa jana Oktoba 21, 2021 kwenye ukumbi wa Mwl JK Nyerere Jijini Dar es salaam. Yanga iliondoka na tuzo 2 ilhali Azam, Coastal na Mbeya City walipata moja.

Baadhi ya wachezaji wa Simba wakishika tuzo zao baada ya kuibuka washindi.

Tuzo iliyokuwa ikisubiriwa kwa hamu ni pamoja na tuzo ya mchezaji bora Ligi kuu ambayo imeenda kwa nahodha wa Simba John Bocco akiwashinda Mukoko Tonombe (Yanga)  na Clatous Chama (Simba).

Utoaji wa tuzo hizo umefanyika mbele ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye usiku huo. Tuzo zote pamoja na vikosi bora vya msimu ni kama zifuatazo:

Mshambuliaji wa Namungo, Reliants Lusajo ametwaa tuzo ya mfungaji bora wa Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC).

Lusajo katika michuano hiyo alifunga mabao manne na tuzo yake imepokelewa na mtendaji mkuu wa Namungo, Omari.Ruvuma Queens imechukua tuzo ya timu yenye nidhamu Ligi Kuu ya Wanawake (SWPL)

Nahodha wa Simba, John Bocco amepata Tuzo ya mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara msimu wa 2020/2021. Katika msimu huo Bocco alifunga jumla ya mabao 16.

Timu ya Coastal Union imeshinda tuzo ya timu yenye nidhamu ikizifunika Mwadui na Simba.

Meneja wa Uwanja wa Nelson Mandela uliopo Sumbawanga, John Zwala ameibuka Meneja Bora wa Uwanja kwa msimu wa 2020/2021.

John amewashinda Sikitu Kitakala (Azam Complex, Dar), na Midestus Mwalukwa (Sokoine, Mbeya).

Kamishina wa mechi, Pili Mlima kutoka Arusha ameshinda tuzo ya tuzo Kamishina bora wa mechi

.Seti bora ya Waamuzi wa msimu uliopita ni ile iliyochezesha mechi kati ya Simba na Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Waamuzi hao ni Ahmed Arajiga, Reonard Mkumbo, Hamdani Said na Hellen Mduma.

Sikudhan Mkulungwa, amepata tuzo ya mwamuzi bora msaidizi kwa Ligi Kuu ya Wanawake

. Amina Kyando Mwamuzi Bora Ligi ya Wanawake Tanzania akiwashinda Tatu Malongo na Esther Adabert.

 Frank Komba Mwamuzi bora msaidizi wa Ligi Kuu Bara na amewashinda Ramadhan Kayoko na Emannuel Mwandemwa.