Jumatatu , 27th Jan , 2020

Mlinda mlango wa klabu ya Yanga, Ramadhan Kabwili ametoa tuhuma nzito kuwa aliwahi kufuatwa na uongozi wa klabu ya Simba wakitaka atafute kadi ili asicheze mchezo wa watani na wampatie gari aina ya IST.

Ramadhan Kabwili

Kabwili amesema hayo alipokuwa akihojiwa katika kipindi cha Kipenga Xtra cha East Africa Radio, Jumatatu, Januari 27, 2020 ambapo amesema kuwa tukio hilo lilitokea wakati Yanga ikiwa na kocha Mwinyi Zahera.

Amesema kuwa siku hiyo Yanga ilikuwa inaelekea kucheza na JKT Tanzania na yeye alikuwa na kadi mbili za njano, hivyo Simba walimfuata na kumuambia kuwa atafute kadi moja ya njano ili akose mchezo uliokuwa unafuatia wa watani wa jadi huku wakimuahidi kumpa IST mpya, wakiamini kuwa angekaa Klaus Kindoki golini wangemfunga kirahisi.

Katika mchezo huo dhidi ya JKT Tanzania, Yanga ilipoteza kwa kufungwa bao 1-0 ambapo Ramadhan Kabwili ndiye alikuwa golikipa wa Yanga siku hiyo.

Aidha Kabwili amesema kuwa kwa sasa ahitaji meneja yoyote atakayemtafutia timu ya Tanzania akitamani meneja ambaye atamtafutia timu Ulaya, "mimi nataka meneja ambaye atanipeleka kucheza soka la Ulaya, sitaki meneja wa kunichezesha hapa nchini kwa sababu kama ni hapa nchini sasa hivi nipo katika klabu kubwa Tanzania na inashinda mataji".