TFF yatoa agizo kwa Dodoma FC

Jumatatu , 12th Feb , 2018

Shirikisho la Soka nchini TFF limeitaka timu ya Dodoma FC kuwa wavumilivu katika kusubiri majibu ya rufaa zao kama wamefuata masharti kwani walitoa nafasi kwa timu zenye malalamiko kuweza kuyawasilisha.

Afisa habari wa TFF Mario Clifford Ndimbo amesema, kanuni walizonazo ni kutotangaza timu iliyopanda Daraja kushiriki Ligi kuu msimu ujao kabla ya saa 72 kukamilika na pia ziliwekwa taratibu za kukata rufaa na kupangwa siku ya kusikiliza.

“Kama Dodoma FC wanasema wamekata rufaa maana yake kunataratibu ambazo zinatakiwa kufuatwa katika ukataji wa rufaa na kama wametimiza itapangwa siku ya kusikiliza, huwezi kukata rufaa leo na  ikasikilizwa leo leo”, amesema.

Aidha Ndimbo amesisitiza kuwa wanasubiri taratibu zote zikamilike ili waweze kutaja timu iliyopanda rasmi kushiriki Ligi kuu kwa msimu wa mwaka 2018/19.

Dodoma FC ilituma malalamiko kwa Bodi ya Ligi wakiwalalamikia wapinzani wao Toto African kumtumia mchezaji ambaye hakuwa na leseni, huku timu za Alliance Schools ya Mwanza na Biashara ya Mara zikiwa zinaongoza kundi C.