Jumapili , 22nd Mei , 2016

Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara VPL imemalizika hii leo katika viwanja mbalimbali hapa nchini na hatimaye kupata majibu ya nani wataungana na Coastal Union kushuka daraja na ni nani wataungana na Yanga katika nafasi nne za juu msimu huu.

Wachezaji wa timu za Mgambo JKT na African Sports wakichuana wakati timu hizo zilipokutana.

Baada ya wagosi wa Kaya kutangulia Daraja la kwanza Tanzania bara FDL msimu ujao kutokana na kushuka daraja kutoka VPL , hii leo wanatanga wengine maafande wa JKT Mgambo FC na wenzao wanakimanumanu timu ya African Sports nazo zimeungana na Wagosi hao kuteremka daraja na kufanya sasa rasmi kuwa timu zote za kutoka jijini Tanga kushuka na hivyo sasa Wanatanga ni wazi wataikosa Ligi Kuu Bara msimu ujao.

Coastal Union, Mgambo Shooting na African Sports zimeshuka daraja baada ya kushika nafasi tatu za mwisho kati ya timu zote 16 zilizoshiriki ligi hiyo msimu huu wa mwaka 2015/2016 uliohitimishwa hii leo kwa timu zote kushuka dimbani katika viwanja tofauti hapa nchini.

Kwa hali hiyo sasa timu zote za Tanga, yaani Mgambo JKT, African Sports na Coastal Union zinaipa mkono wa kwaheri Ligi Kuu Tanzania Bara, na sasa zinatoa nafasi ama zikizipisha timu za maafande wa Ruvu Shooting ya Pwani, Mbao FC ya Mwanza na African Lyon ya Dar es Salaam kushiriki VPL.

Mgambo JKT imemaliza ligi hiyo ikiwa na pointi 28, African Sports 26 na wagosi wa kaya Coastal Union alama 22.

Utamu mwingine wa Ligi Kuu Bara ulikuwa katika kuwania nafasi ya pili ambapo Azam FC wamefanikiwa kuipiku timu ya Simba SC kwa kumaliza katika nafasi ya pili baada ya mechi za mwisho za Ligi hiyo kumalizika hii leo.

Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, JKT Ruvu imeibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Simba SC, mabao yake yakifungwa na Abdulrahman Mussa dakika ya kwanza na 30, wakati la Wekundu wa Msimbazi limefungwa na Nahodha Mussa Hassan Mgosi dakika ya 70.

Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam pia, wenyeji Azam FC wamelazimishwa sare ya 1-1 na Mgambo JKT ya Tanga.

Ramadhani Singano ‘Messi’ alianza kuifungia Azam FC dakika ya 60 kabla ya Fully Maganga kuisawazishaia Mgambo dakika ya 72.

Kwa matokeo hayo, Azam FC inamaliza na pointi 64, ikifuatiwa na Simba SC inayomaliza na pointi 62 katika nafasi ya tatu huku maafande wa Magereza kutoka jijini Mbeya timu ya Tanzania Prisons wao wakiambulia nafasi ya nne kwa alama zao 51 wakifuatiwa na Mtibwa Sugar iliyoshika nafasi ya tano kwa alama 50.

Yanga SC ambayo ilitwaa ubingwa wa Ligi Kuu wiki mbili zilizopita, leo imemaliza kwa sare ya kufungana mabao 2-2 na wenyeji Majimaji Uwanja wa Majimaji mjini Songea hivyo kufikisha pointi 73.

Mechi nyingine za kufunga pazia la Ligi Kuu, wenyeji Toto Africans wamefungwa 1-0 na Stand United Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, Coastal Union wamefungwa 2-0 na Prisons Uwanja wa Mkwakwani, Tanga, Mbeya City imelazimishwa suluhu ama sare ya 0-0 na Ndanda FC, Mtibwa Sugar wameichapa 2-0 African Sport na Kagera Sugar wameshinda 2-0 dhidi ya Mwadui FC.

Ukiondoa mambo mengine ya kiufundi yatakayofanywa na TFF na Bodi ya Ligi TPLB na wataalamu wake kuhusu washindi mbalimbali bora wa ligi hiyo ikiwemo kipa bora, mchezaji bora,timu bora, timu yenye nidhamu, beki bora,na nafasi zingine za kiufundi ni nafasi pekee ya mfungaji bora wa ligi hiyo ndiyo iko wazi haijifichi hii ni baada ya Mchezaji Amis Tambwe wa Yanga ambaye mpaka ligi inahitimishwa hii leo yeye ameibuka na magoli 21 akifuatiwa na Hamis Kiiza wa Simba mwenye magoli 19.