Ijumaa , 12th Oct , 2018

Mwanariadha mashuhuri mstaafu ambaye sasa ni mchezaji wa klabu ya Central Coast Mariners ya nchini Australia, Usain Bolt amefunga mabao mawili hii leo katika mchezo wa kirafiki na kuzidi kuongeza matumaini ya kupata mkataba rasmi wa kudumu kuitumikia klabu hiyo.

Central Coast Mariners imeibuka na ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Macarthur South West United katika mchezo huo wa kirafiki, ambapo Usain Bolt amefunga mabao yake ya kwanza katika mchezo wa kiushindani tangu alipojiunga katika soka.

Mchezaji huyo yupo kwa majaribio katika klabu hiyo ambayo inashiriki ligi kuu ya nchini Australia, endapo atafuzu majaribio hayo atapewa mkataba rasmi tayari kwa kuitumikia klabu hiyo kwenye ligi kuu ya nchini humo 'A-League' inayotarajia kuanza wikiendi hii.

"Ilikuwa ni kitu kikubwa kwangu, nafikiri kufunga bao katika mchezo sahihi kama huu ni kitu kikubwa. Mchezo wako wa kwanza unafunga mabao mawili ni kitu kizuri sana", amesema Bolt.

"Kocha ameniambia, 'Skiliza, utapata nafasi zaidi, utakosa kadhaa na utafunga magoli mengi. Ongeza jitihada zaidi katika mchezo unaofuata' ", ameongeza.

Usain Bolt amefanikiwa zaidi katika riadha kwa kipindi kirefu, ikiwemo kushinda medali nane za Olympic kwenye mbio fupi za mita 100 na 200.