Ijumaa , 29th Jun , 2018

Kuelekea  hatua ya mchujo ya michuano ya Sprite Bball Kings inayotarajiwa kuanza Jumamosi hii, waamuzi wamepewa semina juu ya sheia na kanuni za mashindano hayo ambayo yanafanyika kwa mara ya pili baada ya kuanza mwaka jana.

Waamuzi wa Mpira wa Kikapu ambao wameteuliwa kuchezesha Sprite Bball Kings wakiwa kwenye semina leo.

Semina ya michuano hiyo inayoandaliwa na East Africa Television kwa udhamini wa kinywaji cha Sprite imefanyika kwenye Ofisi za East Africa Television ambapo jumla ya waamuzi 30 walioteuliwa na Chama cha waamuzi wa Mpira wa Kikapu Jijini Dar es Salaam ( DAREDA ) walihudhuria.

Akifafanua kuhusu kanuni hizo Kamishna wa Ufundi na Mipango wa Shirikisho la Mpira wa Kikapu Tanzania (TBF), Manase Zablon amesema kuwa waamuzi wanatakiwa wazingatie muda wa mchezo (Running Time) ambao utakuwa dakika 10 katika nusu ya kwanza na dakika 10 nusu ya pili hivyo kukamilisha dakika  20 za mchezo mzima.

Pia Zablon alisisitiza kwa waamuzi kuhusu suala la umri wa wachezaji na uraia ambapo amesema wachezaji watakaoruhusiwa kucheza ni wenye umri wa kuanzia miaka 16 na kuendelea na wanapaswa kuwa raia wa Tanzania na Sheria zitakazotumika ni za FIBA na kanuni za TBF.

Kutoka kushoto ni Gosbert Boniface (Mkurugenzi wa Ufundi na Mashindano wa Chama cha Mpira wa Kikapu Dar Es Salaam) na Kamishna wa Ufundi na Mipango wa Shirikisho la Mpira wa Kikapu Tanzania (TBF), Manase Zablon.

Naye Mkurugenzi wa Ufundi na Mashindano wa Chama cha Mpira wa Kikapu Dar Es Salaam, Gosbert Boniface aliwaasa waamuzi kuzingatia Sheria na Kanuni hizo na pia kuwa makini na majukumu yao katika michezo hiyo ili kuifanya kuwa na ladha tofauti na ya mwaka uliopita.

Naye Mkuu wa vipindi wa East Africa Radio, Nasser Kingu alimalizia kwa kuwahimiza wadau wa Mpira wa Kikapu Jijini Dar es Salaam na maeneo ya karibu wafike katika viwanja vya JK Park, Kidongo Chekundu ili waweze kujionea Burudani ya kutosha kutoka katika mashindano hayo ambapo pia baadhi ya vipindi vya East Africa Radio vitaruka moja kwa moja kutokea katika viwanja hivyo.