Jumapili , 13th Dec , 2015

Ndoto za wachezaji wa kimataifa wa Tanzania Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu kucheza fainali ya ligi ya klabu bingwa ya dunia nchini Japani ama angalau kukutana na timu kubwa kama Barcelona imeyeyuka baada ya hii leo timu yao kupoteza mchezo.

Wachezaji wa Tanzania Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu wanaokipiga na timu ya TP Mazembe ya DR. Congo.

Mabingwa wa soka wa klabu bingwa barani Afrika timu ya soka ya TP Mazembe imeanza na mguu mbaya michuano ya Kombe la Dunia baada ya kutolewa katika robo fainali ya michuano hiyo ikiwa ni mechi ya kwanza tu kwa kipigo cha mabao 3-0 kutoka kwa Wajapan.

Timu ngumu ya Sanfrecce Hiroshima ndiyo iliyotoa kipigo hicho kwa TP Mazembe ya DR Congo ambayo safu yake ya ushambuliaji inaongozwa na Watanzania Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu.

Kipigo hicho kinafuta ndoto za watanzania hao kufika nusu fainali ya michuano hiyo na kukipiga na River Plate ya Argentina na pia kutinga fainali ya michuano hiyo ama hata ndoto za kucheza na nyota wakubwa wanaotikisa soka barani Ulaya na duniani kwa ujumla kama washambuliaji pacha wa mabingwa wa Ulaya FC Barcelona kina Lionel Mesi, Neymar na Luis Suarez .

Katika mchezo huo mkali wenyeji wa michuano hiyo msimu huu Wajapani walianza kupata bao lao la kwanza katika dakika ya 44 kupitia Yusuke Chajima bao ambalo lilidumu hadi mapumziko.

Sanfrecce walipata bao la pili katika dakika ya 56 lililofungwa na Kazuhiko Chiba akifunga baada ya kuunganisha kona ya Chajima aliyepiga kona iliyozaa bao la kwanza.

Wakati Mazembe wakionekana kupambana kubadilisha mambo hasa baada ya Ulimwengu kuingia katika dakika ya 46, Sanfrecce walifunga bao la tatu katika dakika ya 78 kupitia Asano aliyeunganisha krosi ya Mikic.

Adama Traore na Assale, nusura wafunge kutokana na kujaribu vizuri lakini mwisho mambo hayakuwa mazuri kwa Mazembe.

Sasa Sanfrecce Hiroshima inarudi dimbani Desemba 16 kuwavaa mabingwa wa Amerika Kusini River Plate wanaotokea Argentina.

Nusu fainali nyingine itakuwa siku inayofuata wakati mabingwa wa Ulaya, Barcelona watakapowavaa Guangzhou, kikosi kinachonolewa na Philipe Scolari huku wao Mazembe baada ya kadhia hiyo toka kwa wajapani sasa timu hiyo itamenyana na Club America siku hiyo kuwania nafasi ya tano mchezo utakaopigwa katika uwanja wa Nagai.