Alhamisi , 17th Jan , 2019

Katika kipindi cha miaka kadhaa ambayo Simba haikushiriki michuano ya kimataifa, msemaji wake Haji Manara alikuwa akipambana na Bodi ya ligi (TPLB) juu ya Yanga na Azam FC kuwa na viporo vingi na kufikia hatua ya kusema wanapanga matokeo.

Haji Manara

Hivi sasa mambo yamegeuka na huenda Haji Manara anatamani maneno haya, ''Kama ambavyo Yanga na Azam FC wanapanga matokeo'', yafutike lakini teknolojia imetunza na yanatumika kama kumbukumbu ikimkumbusha kuwa mambo yamegeukia kwake wakati huu ambao Simba ina viporo 7 vya ligi kuu soka Tanzania bara.

Akiwa kwenye moja ya mikutano ya klabu na wanahabari miaka iliyopita Manara alisema, ''Kwa kawaida timu inatakiwa kucheza mechi moja na kupumzika ndani ya saa 72 lakini Bodi ya ligi inatoa maelezo mengi kitu ambacho si sawa''.

Aidha Manara aliweka wazi kuwa Yanga ambayo ilikuwa na viporo 9 ilikuwa inapanga matokeo kwa kutumia mfumo wa 'Indirect' kwani kuna baadhi ya timu ambazo zilikuwa zinakaribia kushuka daraja huenda zisingekuwa na ushindani wakati ambao zitacheza na Yanga.

Hata hivyo kwa upande wa pili ambao ni Yanga na Azam FC msimu huu wao wapo kimya na hawajalalamika licha ya Simba kupumzika kwa zaidi ya saa 72 lakini imekuwa haichezi mechi zake za ligi na kuendelea na maandalizi ya michuano ya kimataifa.