Yanga wafafanua tiketi zao kuingiliana na Simba

Ijumaa , 9th Aug , 2019

Uongozi wa klabu ya Yanga umefafanua juu ya mkanganyiko uliojitokeza katika mchezo wa kilele cha Wiki ya Mwananchi, Agosti 4 ambapo tiketi za mashabiki ziliingiliana na tiketi za mchezo wa watani wao Simba.

Dismas Ten (kulia) na baadhi ya viongozi wengine

Akielezea hilo katika mkutano na wanahabari Makao Makuu ya Yanga hii leo kwa niaba ya Yanga, mwakilishi wa kampuni ya Salecom inayouza tiketi katika Uwanja wa Taifa amesema kuwa waliweka mechi mbili katika mfumo ili kuwawezesha mashabiki wa timu zote kununua tiketi kwa urahisi ambapo muda uliowekwa ulipoisha, tayari mechi iliyofuata ikaanza kuonesha tiketi zake.

"Huu mfumo upo kidigitali kwahiyo mechi ya Yanga tulipewa 'kick-off' ya saa 5 kwa maana ya shughuli kuanza kwahyo huwa tunahesabu masaa mawili kwa mchezo kumalizika ndio maana ilipofika saa 7 mfumo ukaanza kuonesha tiketi za mchezo unaofuata kwa kuwa ulishapima kuwa mchezo wa kwanza umemalizika", amesema.

"Lakini kwa kile kipande kidogo kilichoonesha tiketi za mchezo unaofuata, ambapo baada ya kugundua tukarekebisha na mapato yaliyoingia katika mchezo huo yakarudhishwa", ameongeza.

Aidha Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga, Dismas Ten amesema kuwa klabu hiyo imejiandaa vya kutosha kuelekea mchezo wa Klabu Bingwa Afrika dhidi ya Towship Rollers kesho Jumamosi, huku akiwataka mashabiki kujitokeza kwa wingi uwanjani kama walivyofanya kwenye kilele cha Wiki ya Mwananchi.