'Yanga wananiogopa, wanatamani' - Haji Manara

Ijumaa , 3rd Jan , 2020

Msemaji wa klabu ya Simba Haji Manara, amesema mashabiki wa Yanga wanamugopa sana, wanatetemeka na wengine wanatamani hadi afe pale wamuonapo ila ndiyo hivyo hawana cha kumfanya.

Msemaji wa klabu ya Simba, Haji Manara.

Akipiga stori na EATV & EA Radio Digital, Haji Manara amesema hayo baada ya baadhi ya mashabiki wa klabu ya Yanga kumsema kwamba anaropoka sana.

"Nitajie neno moja ambalo unaona nimeropoka, baadhi ya mashabiki wa Yanga ndiyo wanasema naropoka sio watu, tena wanaotoka mitandaoni wapuuzi wanasema mimi naropoka sasa si ningekamatwa na polisi yaani niropoke halafu Serikali iniache, Yanga huwa wanajiona  wakubwa na hawaguswi wanataka wawatanie Simba halafu wao wasitaniwe" amesema HajiManara.

Haji Manara ameongeza kuwa "Vyote ninavyoongea nina uhakika navyo hakuna hata kimoja nisichokuwa na uhakika, tangu nimeanza kuwa boksi Yanga wananiogopa halafu hawana cha kunifanya hata nikitokea wanatetemeka na wengine wanatamani nife".

Siku ya Januari 4, 2020, kutakuwa na mchezo wa ligi kuu kati ya timu yake ya Simba dhidi ya watani wao wa jadi Yanga, utakaochezwa majira ya saa11:00 jioni, katika uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.