Jumanne , 24th Dec , 2019

Kikosi cha klabu ya soka ya Yanga kipo katika wakati mzuri kuelekea mchezo wa ligi kuu soka Tanzania Bara dhidi ya Mbeya City, ambapo mazoezi ya mwisho yaliyofanyika jana kwenye uwanja wa Sokoine yalimalizika salama na wachezaji wote wapo vizuri.

Wachezaji wa Yanga (kushoto) na mchezaji wa Mbeya City (kulia) akipatiwa matibabu baada ya kujeruhuiwa Jumamosi.

Yanga imethibitisha hilo kwa kuweka wazi kuwa, 'Kikosi cha Mabingwa wa Kihistoria kimefanya mazoezi ya mwisho kwenye Uwanja wa CCM Sokoine jijini Mbeya na kipo tayari kwa mchezo wa VPL dhidi ya Mbeya City'.

Kwa upande wa wenyeji wao ambao ni Mbeya City, mambo si mazuri sana kutokana na baadhi ya wachezaji wao kuwa na majeraha yaliyotokana na vurugu zilizotokea Jumamosi Disemba 21, 2019 baada ya mchezo wa Kombe la shirikisho dhidi ya Migombani FC.

Wachezaji kadhaa wa Mbeya City walishambuliwa na kujeruhiwa na mashabiki wa Migombani FC hivyo kuwasababishia kupata majeraha na maumivu katika sehemu mbalimbali za mwili.

Miongoni mwa walioumizwa siku hiyo ni meneja wa timu hiyo Mwagane Yeya na hali yake inaendelea vizuri pamoja na wachezaji wengine waliojeruhiwa.

Yanga inakwenda kucheza na Mbeya City ikiwa na pointi 17 katika nafasi ya 8 baada ya mechi 8. Wakati Mbeya City ina alama 8 katika mechi 12 ikiwa nafasi ya 19 kwenye msimamo wa ligi.