Jumatano , 30th Mar , 2016

Michuano ya kombe la Shirikisho (Federation Cup) inatarajiwa kuendelea kesho Alhamisi kwa michezo miwili kuchezwa katika hatua ya robo fainali ya michuano hiyo, michezo yote hiyo ikipigwa jijini Dar es Salaam katika viwanja tofauti.

Kikosi kamili cha timu ya soka ya Yanga ya jijini Dar es Salaam.

Michuano ya Kombe la Shirikisho (Federation Cup) inatarajiwa kuendelea leo Alhamisi kwa michezo miwili kuchezwa katika hatua ya robo fainali ya michuano hiyo, michezo yote hiyo ikipigwa jijini Dar es Salaam katika viwanja tofauti.

Michezo itakayopigwa jijini Dar es Salaam itazikutanisha timu za Azam FC ambao ni wawakilishi wa Tanzania katika michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika, watakao kuwa kwenye uwanja wa Azam Complex kuwakaribisha maafande wa Tanzania Prisons kutoka jijini Mbeya katika mchezo ambao kambi za timu zote mbili zimekiri ugumu na upinzani mkali katika muda wote wa mchezo huo. utakaoanza mida ya saa 10 jioni kwa saa za Afrika Mashariki.

Mchezo mwingine utawahusisha mabingwa watetezi wa ligi kuu ya soka Tanzania bara Yanga SC ambao pia ni wawakilishi wa Tanzania katika michuano ya Klabu Bingwa barani Afrika wao watakua wenyeji wa Ndanda FC kutoka mjini Mtwara katika mchezo utakaofanyika ndani ya uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam, huku kila timu ikihitaji ushindi katika michezo hiyo ili kuweza kufuzu kwa hatua ya nusu fainali.

Mchezo wa mwisho wa hatua ya robo fainali utapigwa Aprili 11,wakati vinara wa ligi kuu ya soka Tanzania bara Simba SC watakapokamilisha hatua hiyo kwa kucheza na Wagosi wa Kaya timu ya Coastal Union kutoka jijini Tanga mchezo ambao pia utapigwa katika uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Mpaka sasa ni wachimba madini kutoka Shinyanga timu ya Mwadui FC ndio timu pekee ambayo imeshafuzu kwa hatua ya nusu fainali, baada ya kuwachapa Geita Gold kwa mabao 3 -0.

Na kwa mujibu wa taratibu za michuano hiyo kwa hapa nchini ni kwamba timu hizo zikienda sare ya aina yoyote katika muda wa kawaida wa dakika 90 basi mshindi atapatikana kwa njia ya changamoto ya mikwaju ya penati.

Bingwa wa michuano ya Kombe la Shirikisho atawakilisha Tanzania mwakani kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika (CAF CC) mwaka 2017.