Hussein Itaba akijifua tayari kumkabili Tamba jumamosi.
Mabondia chipukizi wa ngumi za kulipwa nchini Hussein Itaba na Ibrahim Tamba wanataraji kushuka ulingoni katika mchezo wa kuwania pigano la kimataifa dhidi ya mshindi kati ya bondia kutoka Ujerumani na mwingine kutoka Thailand.
Mpambano baina ya mabondia hao chipukizi wanaotoka kitongoji cha Manzese jijini Dar es Salaam umekuwa gumzo kutokana na upinzani wa mabondia hao ambao unachangiwa na ubora wa mabondia wote wawili.
EATV Michezo imetembelea Kambi ya bondia Hussein Itaba ili kufahamu maandalizi yake kuelekea mpambano huo ambapo pia ilikutana na mratibu wa pambano lenyewe Doto Texas.
Akizungumzia mpambano huo huku akipata sapoti kubwa ya kuungwa mkono na kocha wake Mohamed Waziri bondia Hussein Itaba amesema hatarajii kupata upinzani mkubwa kwa bondia Ibra Tamba na kimsingi ametamba kumwangushia kichapo kizito bondia huyo halikwepeki na atakachofanya ni kumchelewesha kwa mizunguko miwili [raundi mbili] na baadaye kumlaza chini kwa makonde mazito kwa pigo la Knock out[KO].
Naye Mratibu wa mpambano huo Doto Texas amesema maandalizi ya mpambano huo ambao utatanguliwa na mapambano matano ya utangulizi yamekamilika kwa asilimia kubwa na kimsingi pamoja na upinzani baina ya mabondia hao lakini ushindani unazidishwa kutokana na kuwepo kwa nafasi ya kupata pambano kubwa la kimataifa la uzito wa kati ambao ndio watashindania mabondia hao kwa mizunguko 12.