Ijumaa , 7th Oct , 2016

Serikali imeshauriwa kuanzisha mifumo rasmi ya kutoa taarifa dhidi ya matukio ya ukatili kwa wanafunzi yanayoendelea katika shule nchini.

Mtendaji wa Shirika la Haki Elimu nchini Bwana John Kalage.

Mifumo hiyo ni ili kuwawezesha wanafunzi na wadau wengine kutoa taarifa kwa vyombo husika pindi wanapokutana na matukio ya kikatili katika maeneo yao kwa lengo la kuyakomesha.

Rai hiyo imetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Haki Elimu, Bw. John Kalage wakati akitoa tamko kuhusu vitendo vya ukatili vinavyoendelea kutokea mashuleni kama kipigo cha kikatili alichopata mwanafunzi Sebastian Chinguku wa Kidato cha 3 katika Shule ya Sekondari ya kutwa ya Mbeya.

Bw. Kalage ameishauri serikali kuhakikisha miongozo yake ya kusimamia na kuimarisha nidhamu mashuleni inazingatiwa na watu wote sawia na kuangalia upya utaratibu wa uchaguzi na uandaaji wa waalimu katika vyuo mbalimbali vinavyotoa mafunzo ya ualimu hapa nchini.

Kwa upande wa wanafunzi Bw. Kalage amewataka wawajibike na kuhakikisha kuwa wanaheshimu walimu wao pamoja na walezi kwani ukosefu wa nidhamu kwa wanafunzi husababisha hali ya kutokuwa na maelewano na upendo baina ya walimu na wanafunzi.

Ripoti ya utafiti ya UNICEF kuhusu ukatili dhidi ya watoto ya mwaka 2011 imeonesha kuwa kuna viwango vya kutisha vya ukatili dhidi ya watoto katika shule nyingi nchini vikiwemo vya kimwili, kingono na kihisia katika mazingira ya shule za Tanzania na kwamba walimu ndiyo vinara wa ukatili huo.

Kwa mujibu wa utafiti huo zaidi ya nusu ya wasichana na wavulana ambao wamewahi kunyanyaswa kimwili, kwa kufinywa, kuchapwa viboko na mateke, waliwataja walimu kuwa ndiyo wanyanyasaji wakuu shuleni nchini Tanzania.

Ripoti hiyo ilibainisha kuwa, kwa kiasi kikubwa matukio kama haya yamezifanya shule kutokuwa sehemu rafiki na salama kwa wanafunzi na hivyo kuwa na athari kubwa katika juhudi zao za kujifunza, adhabu kama hizi zinapotolewa kwa watoto, husababisha mtoto kutafuta namna ya kukwepa adhabu hizo na ndipo huanza kukosa shule mara kwa mara na hatimaye kuamua kuacha shule kabisa.