Ijumaa , 7th Oct , 2016

Mikoa zaidi ya 10 imejitokeza kushiriki katika Mashindano ya Klabu Bingwa ya Ngumi Taifa yanayotarajiwa kuanza kutimua vumbi Oktoba 09 mwaka huu jijini Dar es Salaam huku Kenya ikiwa mgeni mwalikwa katika mashindano hayo.

Pambano la ngumi

Rais wa Chama Cha Ngumi Tanzania BFT Mutta Lwakatare amesema, ndani ya mashindano hayo pia kutakuwa na uzinduzi wa mashindano ya ngumi za ridhaa yaliyosajiliwa na Shirikisho la Ngumi Duniani AIBA ambayo yatawasaidia mabondia wa ngumi za ridhaa kujipatia kipato ndani ya mchezo huo tofauti na ilivyokuwa hapo awali.

Lwakatare amesema, mabondia wote wa Ngumi za Ridhaa kwa sasa watakuwa wakisajiliwa na BFT ili kujihakikishia wanapata mapato halali na watakuwa wakipata fursa za kupigana ngumi katika nchi mbalimbali nje ya Tanzania.

Mikoa iliyohakiki ushiriki wa mashindano hayo ni Tanga, Kigoma, Morogoro, Pwania, Iringa, Mbeya, Tabora na wenyeji Dar es Salaam huku Kenya ikileta vilabu vitatu ambapo kimoja ni kutoka mjini Mombasa na viwili vikitokea jiji la Nairobi.