Ijumaa , 7th Oct , 2016

Timu 12 zinatarajiwa kushiriki Ligi ya Taifa ya Wanawake inayotarajiwa kuanza Novemba mosi, mwaka huu kwa mujibu wa taarifa ya Kamati ya Maendeleo ya Soka la Wanawake na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), zilizoridhia tarehe hiyo.

Rais wa TFF Jamal Malinzi (Kushoto) akiwa na Mwenyekiti wa Chama cha Soka la Wanawake

Tayari klabu zimeagizwa kuzingatia jina kuendana na namba za jezi mgongoni ili kuepusha mkanganyiko wa wachezaji wakati wa ligi hiyo inayofanyika kwa mara ya kwanza nchini Tanzania.

Timu 12 zinatarajiwa kushiriki ligi hiyo ambapo kesho Oktoba 8, 2016 itakuwa ni siku ya kuchambua fomu za usajili wakati Oktoba 10, mwaka huu majina ya usajili yatatangazwa pia klabu zitatumiwa kupitia anwani za barua pepe.

Kwa mujibu wa taarifa ya TFF iliyotolewa leo kwa vyombo vya habari, Oktoba 11 na 12, 2016 ni muda wa klabu kupeleka mapingamizi yatakayosikilizwa Oktoba 15, mwaka huu.

Imesema kuwa majina ya pingamizi yatatangazwa kabla ya Oktoba 20, 2016 huku maandalizi ya ligi yataendelea.

Pia TFF imezitaka klabu kutangaza aina ya rangi wanazotumia katika michezo ya nyumbani na ugenini na kutakiwa kusafiri na jozi zote mbili ili kuepuka mkanganyiko wa kufanana jezi.

Kutakuwa na jopo la makocha watakaofanya uteuzi wa wachezaji nyota watakaoitwa kwenye timu za taifa ambaye atagharamiwa na TFF.

Vyama vya mikoa vimetakiwa kusaidia klabu katika bajeti zao kwa vile tathmini inaonesha kuwa fedha zinazotoka hazitoshi pamoja na kusaidia maandalizi ya michezo kama vile kuandaa uwanja.

Taarifa hiyo pia imeweka wazi kuwa hakutakuwa na zawadi ya fedha zaidi ya kombe la medali kwa timu shiriki.

Pia hapakutakuwa na zawadi kwa mchezaji bora, mfungaji bora, kipa bora, ingawa kutakuwa na jopo la kuwachagua.

Mchezaji bora atachaguliwa kwenye hatua za mwisho wa mashindano, mfungaji bora atachaguliwa kuanzia hatua ya kwanza ya mashindano.