Jumatatu , 10th Sep , 2018

Mlinda mlango wa Taifa Stars, Aishi Manula ametoboa siri ya ujasiri aliokuwa nao kuwazuia Uganda kufunga katika mchezo wa kufuzu AFCON uliofanyika nchini humo wikiendi iliyopita.

Manula

Katika mchezo huo, Uganda ‘Cranes’ walionekana kushambulia mara nyingi lango la Stars hasa katika kipindi cha kwanza lakini uimara wa mabeki pamoja na kipa, Aishi Manula uliisaidia Stars kutoruhusu bao lolote.

Akizungumza mara baada ya kurejea nchini kutokea nchini Uganda, mlinda mlango huyo namba moja wa Taifa Stars, amesema,

"Mimi nadhani mpaka mpaka sasa hapa nilipofikia sio kwamba ni kijana sana, ni mechi nyingi nimecheza na kwenye timu ya taifa pia niko muda mrefu, kwahiyo kuna michezo mingi ya aina hiyo nimekutana nayo. Ni vitu vya kawaida sana kwangu, ni kujiamini tuu na vitu kama vile mara nyingi vinatokea katika mechi za ugenini".

Mlinda mlango huyo namba moja wa Taifa Stars anaamini wanayo nafasi ya kufanya vizuri katika michezo ijayo licha ya kwamba Uganda ndiyo timu inayopewa nafasi kubwa ya kufanya vizuri katika kundi hilo.

Taifa Stars iko katika kundi ‘L’ ikiwa pamoja na timu ya taifa ya Uganda, Cape Verde na Lesotho. Uganda inaongoza kundi hilo ikiwa na alama 4 baada ya kushinda mchezo mmoja na kutoka sare mchezo mmoja ikifuatiwa na Lesotho yenye alama mbili, Stars nayo ina alama mbili huku Cape Verde ikiburuza mkia kwa alama moja katika michezo miwili iliyocheza.