Ijumaa , 1st Mar , 2019

Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) limetangaza kusitisha usajili wa Msanii, Godfrey Tumaini (Dudubaya) kuanzia jana Februari 28, kutokana na utovu wa nidhamu.

Dudu Baya

Kupitia barua iliyosainiwa na Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) Godfrey Mngereza amesema kuwa baraza limechukua hatua hizo baada ya msanii huyo kukamatwa na jeshi la polisi kutokana na kauli zake kwenye mitandao ya kijamii.

"Dudu Baya amekuwa anatoa kauli zisizofaa kwenye mitandao ya kijamii hivi karibuni, hivyo BASATA linasisitiza kuwa msanii anaposajiliwa hutakiwa kuwa raia mwema na mfano wa kuigwa na jamii kwani msanii ni kioo cha jamii", amesema Mngereza.

Mngereza ameongeza kuwa wasanii wote wanatakiwa kutokiuka taratibu na sheria zilizopo ili kujiepusha kuingia katika migogoro isiyo ya lazima na Baraza hilo.

Dudu Baya anashikiliwa na Jeshi la Polisi katika kituo cha Osterbay jijini Dar es salaam kwa kosa la kutoa maneno ya kumdhihaki marehemu Ruge Mutahaba katika mitandao ya kijamii.