Jumanne , 17th Nov , 2020

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Sekta ya Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah amesema serikali nchini imefanikiwa kudhibiti uvuvi haramu kwa kutumia mabomu nchini ndani ya mwaka mmoja.

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Sekta ya Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah

Akizungumza katika ziara yake ya siku moja ya kwenda kuangalia ujenzi wa ofisi za BMU Kata ya Kipumbwi, Pangani Dkt. Rashid alisema kuwa udhibiti wa uvuvi haramu amabo umefanywa na serikali,watu wanaoitakia mema nchi pamoja na taasisi za ulinzi na usalama umesaidia katika kuongeza upatikanaji wa samaki wanaozalishwa nchini.

“Serikali iliamua kuchukua hatua za makusudi na kuanzisha operesheni za uvuvi haramu kwenye maziwa waliziita operesheni sangara na operesheni jodari ambazo ziliwasaidia hivyo baada ya mwaka mmoja matokeo yalikuwa mazuri sana kwenye ukanda wa pwani ikiwemo maeneo ya Kigombe na Tanga kwani uvuvi wa mabomu ulikuwa umekithiri kule Dar mabomu yalikuwa yakipigwa mpaka pale karibu na Ikulu” Alisema Dkt. Rashid

Aidha Dkt.Tamatamah, amesema kwa upande wa maziwa akizungumzia ziwa Viktoria alisema serikali imefanikiwa kutokemeza uvuvi haramu wa matumizi ya nyavu haramu kwa asilimia 80.

Hata hivyo Dkt.Tamatamah amesema kuwa katika kipindi cha awamu ya tano wametoa elimu na wavuvi haramu wengi wamebadilika na kuipa nguvu serikali kwa kipindi hiki cha pili wajikite kwenye ujenzi wa viwanda vya kuchakata samaki na kuwawezesha watu kiuchumi ili wawekeze kwenye maeneo yote kuvua.