Jumatano , 30th Dec , 2020

Michezo miwili ya ligi kuu nchini England ipo kwenye hati hati ya kughairishwa, kwasababu maambukizi ya ugonjwa wa korona nchini humo yamezidi kushika kasi na kufikia visa 18, ambavyo ni vingi zaidi kuripotiwa ndani ya siku  moja.

Joel Matip wa Liverpool akiwania mpira na Ivan Cavaleiro wa Fulham kwenye mechi ya EPL

Michezo ambayo ipo kwenye hati hati ya kughairishwa ni wa Tottenham Hotspurs ambao wapo kwenye dimba lake la nyumbani kuikaribisha Fulham saa 3:00 usiku na Majogoo wa jiji Liverpool kukipiga ugenini kwa Newcastle United saa  5:00 usiku wa leo tarehe 30 Disemba 2020.

Mashaka ya michezo hiyo kughairishwa yanakuja baada ya Kocha wa Fulham Scott Parker kupatwa na ugonjwa huo licha ya kupona lakini mashaba yamesalia kwa afya za wachezaji alioingiliana nao wakati kwa upande wa Newcastle, Jamal Lascelles na Allan Maximin, bado wanasumbuliwa na Korona.

Licha ya hofu ya michezo hiyo kughairishwa lakini vilabu hivyo vimeendelea na utaratibu wa kawaida wa kufanya mahojiano na wanahabari na kutoa taarifa ya hali ya vikosi, ambapo Spurs wanatazamiwa kuwakosa Giovani Lo Celso, Lucas Moura na Gareth Bale wenye majeraha.

Fulham wamethibitisha kocha wake Scott Parker amepona na kumaliza kujitenga kwa siku 10 hivyo atarejea benchini, Mario Lemina na Kenny Tete watarejea baada ya kukosa mchezo uliopita dhidi ya Southampton kwa sababu za kifamilia.

Kwa upande mwingine, Liverpool imethibitisha kuwakosa Joel Matip, Naby Keita na Thiago Alcantara ambao wanaendelea kusumbuliwa na majeraha ya mara kwa mara wakati Newcastle Utd ambao wameripoti visa kadhaa wataendelea kuwakosa Jamal Lascelles na Allan Maximin.

Wazo la kusimamisha michezo ya EPL ili kukwepa uwezekano wa kueneza maambukizi hayo kwa kasi zaidi linaungwa mkono na baadhi ya madaktari waliopo kwenye jopo la madaktari wa ligi hiyo na tayari michezo 9 ya Champions na ligi za chini imesimamishwa usiku wa jana.