Ijumaa , 2nd Apr , 2021

Golikipa wa Namungo Jonathan Nahimana amesema ni lazima washinde katika mchezo wao ujao wa kombe la shirikisho dhidi ya Nkana FC ya Zambia, utakao fanyika katika uwanja wa Mkapa jijini Dar-es-Salaam Jumapili hii.

Kikosi cha Namungo ya Ruangwa Lindi

''Ni lazima tushinde mchezo huu ili kuendelea kubaki kwenye ushindani ndani ya kundi letu, ratiba yetu haikuwa rafiki nasi, tumeanza na timu kubwa zilizofanikiwa kisoka kwenye ligi zao za ndani pamoja na ushiriki wao kwenye michuano mbalimbali ya CAF,'' alisema Nahimana.

''Tunawaona kama Nkana ni saizi yetu kwa kila hali, kwanza ukanda wanaotoka na wetu hatujapishana sana tamaduni. Uwekezaji wa timu zetu unajulikana, hivyo hatuoni sababu za wao kutufunga hapa nyumbani'' aliongeza Nahimana.

Nahimana ambaye ni mchezaji wa kimataifa raia wa Burundi, aliyejiunga na timu ya Namungo akitokea KMC ya manispaa ya Kinondoni, amekuwa nguzo muhimu sana katika mafanikio ya timu hiyo akiwa na rekodi nzuri za kudaka penalti katika michuano hii.

Namungo walianza kampeni yao ugenini nchini Morocco, wakapoteza 1-0 dhidi ya Raja Casablanca, wakapoteza tena mchezo wa pili nyumbani dhidi ya Pyramids ya Misri.