Jumatatu , 6th Feb , 2023

Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), limewataka wataalamu wote wa mchezo huo kuwasilisha taarifa zinazoonyesha fani zao.
Agizo hilo, limetolewa na Kaimu Katibu Mkuu RT, Wakili Jackson Ndaweka, ambako amewataka makatibu wa vyama vya riadha mikoa yote ya Tanzania Bara.

Wakili Ndaweka,amesema RT inakusudia kuendesha kozi mbalimbali za kuboresha uwezo wa wataalamu wa mchezo wa riadha waliopo na kuzalisha wengine katika fani ambazo zina upungufu. 

"Ili mpango huu uweze kutekelezeka kwa ufanisi, ni lazima kuwa na taarifa za wataalamu wa Riadha nchini, zitakazowezesha kuainisha maeneo yenye upungufu na kuyawekea mpango maalum," alisema na kufafanua. 

Taarifa zinazotakiwa zinapaswa kuwasilishwa kupitia wasifu 'CV', ambayo inapaswa kuambatanishwa na vivuli vya vyeti vya elimu ya Riadha na elimu ya kawaida. 

Wakili Ndaweka, alisema takwimu hizo ni muhimu sana kwa maendeleo ya mchezo wa riadha nchini. 

"Makatibu wanapaswa kuwajulisha wataalam waliopo kwenye mikoa yao, wawasilishe taarifa hizo kupitia anuani ya barua pepe ya shirikisho ambayo ni [email protected] si zaidi ya tarehe 20/02/2023," alisisitiza Ndaweka.