
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega
Akizungumza bungeni hii leo Mei 3, 2023, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega, amewaomba wabunge kuendelea kushikamana ili kuhakikisha kwa pamoja wanatatua changamoto mbalimbali zikiwemo zile zinazowakabili wakulima na wafugaji.
Jumla ya wabunge 54 walitoa hoja na michango mbalimbali kuhusu wizara hiyo, huku Waziri Ulega akisema kuwa kuhusu suala la uwekaji wa hereni kwenye ng'ombe limeshafanyiwa tathmini na kwamba mawazo yote ya wabunge kuhusu uboreshaji wa zoezi hilo litakaloenda kuinua uchumi wa wafungaji na Taifa kwa ujumla yatafanyiwa kazi.
Aidha akizungumzia mashamba ya serikali yaliyogeuka kuwa mapori makubwa amesema, "Nimesema katika bajeti kwamba, tumetenga fedha za kuhakikisha mashamba yanayomilikiwa na serikali ambayo kwa kiasi kikubwa yamekuwa mapori, tutayafanya mashamba yale yawe ya uwekezaji na uzalishaji ili yaweze kuwa na tija kwa Taifa letu".
Katika hatua nyingine wizara ya hiyo imeshauriana kuzalisha mahindi ya njano ambayo yatakuwa ni uhakika wa chakula cha kuku na mifugo mingine, na kwamba Wizara hiyo inafikiria kuanza zoezi la umwagiliaji wa nyasi ili kuwa na uhakika wa malisho ya ng'ombe hapa nchini.