Jeshi la Polisi Mkoani Dodoma limethibitisha kutokea kwa ajali iliyohusisha lori aina ya FAO Tipa lenye namba T 824 DTS katika eneo la Makulu, ambalo liligonga madereva wa bodaboda waliokuwa kituoni na kusababisha vifo vya watu watano, huku tingo wa lori hilo akijeruhiwa na kupelekwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma kwa matibabu.
Kamanda Polisi wa Mkoa wa Dodoma, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Galus Hyera amesema wanaendelea kumsaka dereva wa lori hilo ambalo liliacha barabara na kusababisha ajali hiyo kisha akatokomea pasipojulikana.
Awali, mashuhuda wameeleza kuwa lori hilo lilikuwa likitokea upande wa UDOM kuelekea katikati ya jiji kabla ya kushindwa kukata kona katika mteremko wa eneo hilo baada ya mpira wa breki kupasuka na kupoteza muelekeo kisha kuwavamia madereva wa bodaboda waliokuwa wamepaki kituoni, pamoja na mteja aliyekuwa dukani.
Miili ya marehemu imehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma huku taratibu za uchunguzi na hatua zaidi zikiendelea.



