Maelfu ya waombolezaji wamejitokeza jijini Goma Mashariki ya DRC, siku ya jana Alhamisi, Januari 8, kuhudhuria ibaada ya mazishi ya watu 22 waliouawa wakati wa mapigano ya hivi karibuni kati ya jeshi la FARDC na waasi wa M23.
Wakati familia za waliouawa zikigubukiwa na huzuni kutokana na uzito wa kuwapoteza wapendwa wao katika mapigano hayo, mapigano yameendelea kushuhudiwa katika Mji wa Masisi ambapo wanajeshi wa DRC wamekuwa wakipambana waasi wa M23 wanaodhibiti mji wa Goma na Bukavu tangu mwaka uliopita.
Jeshi la DRC FARDC na waasi wa M23 wamekuwa wakiendelea kupigana licha ya makubaliano ya kusitisha mapigano.
Umoja wa Mataifa na serikali ya Kinshasa wanaituhumu Rwanda kwa kuwaunga mkono waasi hao wa M23 madai ambayo Kigali imeendelea kukanusha.
Mbali na mauaji, machafuko mashariki ya Kongo yamesababisha mamia kwa maelfu ya raia kukimbia makazi yao, hali ambayo imefanya hali ya kibinadamu kuwa mbaya.



