Monday , 17th Dec , 2018

Mbunge wa Jimbo la Singida Kaskazini, Justine Monko kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) ametaja sababu ya wagombea Ubunge wa CCM, kuchaguliwa na wananchi wachache kwenye chaguzi za marudio kuwa ni kutokana na wananchi kuwa na uhakika na wagombea wa Chama hicho kwamba watashinda.

Mbunge wa Jimbo la Singida Kaskazini, Justine Monko na Lazaro Nyalandu.

Akizungumza na www.eatv.tv Mbunge huyo ambaye alipata nafasi ya kugombea jimbo hilo baada ya kujiuzulu kwa aliyekuwa Mbunge wake Lazaro Nyalandu amesema licha ya kuchaguliwa na wananchi wachache lakini anapewa ushirikiano wa kutosha.

"Changamoto jimboni kwangu ziko nyingi, japo kuna tofauti ya kiutendaji kati yangu na Mbunge aliyepita, kuhusu wapiga kura kujitokeza wachache kunichagua, ni kawaida kwa sababu wananchi wengiinapofka kwenye uchaguzi mdogo huwa wanajiuliza niende au nisiende kupiga kura."

"Ila nikueleze kwa muda niliyokuwa Mbunge, muitikio wa wananchi ni mkubwa, na wamenipa nafasi nzuri sana ya kufanya kazi bila kuwaangalia watu wanaonipinga." ameongeza Mbunge Monko.

Oktoba 30 mwaka jana Lazaro Nyalandu alitangaza kujivua nyadhifa zake zote ndani ya Chama Cha Mapinduzi na kumfanya kukosa sifa za kuwa Mbunge wa chama hicho, ambapo baadaye kutangaza kujiunga na Chama Cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA.