
Kamanda wa Polisi mkoa wa Mbeya Dhahir Athuman Kidavashari amesema wamepokea taarifa ya tukio la kifo cha mfanyakazi wa kiwanda cha SIKA kilichopo maeneo ya Rungwe Mkoani Mbeya,kifo ambacho kimesababishwa na mashine yakusagia kokoto.
Kamanda Kidavashari ameyasema hayo kwenye mahojiano maalumu na East Africa Radio na kusema kuwa marehemu alikuwa anafanya usafi kwenye mashine hiyo yakusaga kokoto, na ghafla kwa bahati mbaya alikanyaga swichi yakuwashia mashine hiyo ndipo ikawaka na kumshinda nguvu na kumvuta ndani ya mashine na kuanza kumsagasaga hadi kufa.
Amesema kuwa niwajibu kwa wafanyakazi na wamiliki wa viwanda kuzingatia sheria za usalama mahala pa kazi kwa kuvaa vifaa vyakuzuia majanga pindi wafanyapo shughuli zao za kila siku ili kuepusha majanga kama hayo yasiendelee kutokea.
Taratibu za maziko ya mtu huyo zinafanywa na wamiliki wa kiwanda hicho kwa kushirikiana na familia ya marehemu na jeshi la polisi mkoani humo litahakikisha usalama wa raia unazingatiwa.